24Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la Bwana Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.” Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.”
25Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.”
26Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa. Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga.
27Wakati wa adhuhuri, Eliya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.”
28Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja wenyewe kwa visu na vyembe, mpaka damu ikachuruzika.