2Kwa hiyo Eliya akaenda kujionyesha kwa Ahabu. Wakati huu njaa ilikuwa kali sana katika Samaria,
3naye Ahabu alikuwa amemwita Obadia ambaye alikuwa msimamizi wa jumba lake la kifalme. (Obadia alimcha Bwana sana.
4Wakati Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Bwana, Obadia alikuwa amewachukua manabii mia moja na kuwaficha katika mapango mawili, hamsini kwenye kila moja na akawa akiwapa chakula na maji.)
5Ahabu alikuwa amemwambia Obadia, “Nenda katika nchi yote kwenye vijito vyote na mabonde. Huenda tunaweza kupata majani ya kuwalisha farasi na nyumbu wapate kuishi ili tusilazimike kuwaua hata mmoja wa wanyama wetu.”
6Kwa hiyo wakagawanya nchi waliyokusudia kutafuta majani, Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.