4Mfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali pa juu pa kuabudia, naye Solomoni akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hayo madhabahu.
5Bwana akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”
6Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.
7“Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu.
8Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao.