9Amazia akamuuliza yule mtu wa Mungu, “Lakini itakuwaje kwa zile talanta 100 za fedha nilizolipa kwa ajili ya haya majeshi ya Israeli?” Yule mtu wa Mungu akajibu, “Bwana aweza kukupa zaidi sana ya hizo.”
10Hivyo Amazia akayaondoa yale majeshi yaliyokuwa yamekuja kutoka Efraimu na kuyarudisha nyumbani. Waliwakasirikia sana Yuda, nao wakarudi nyumbani wakiwa na hasira kali.
11Ndipo Amazia akajitia nguvu na kuliongoza jeshi lake kwenye Bonde la Chumvi, ambako aliua watu 10,000 wa Seiri.
12Jeshi la Yuda pia likawateka watu 10,000 wakiwa hai, likawapandisha juu ya jabali na kuwatupa chini kwa nguvu hata wote wakavunjika vipande vipande.
13Wakati huo yale majeshi Amazia aliyoyarudisha na ambayo hakuyaruhusu kushiriki katika vita, yalivamia miji ya Yuda kuanzia Samaria hata Beth-Horoni. Yakawaua watu 3,000 na kuchukua kiasi kikubwa sana cha mateka.