3Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana, lakini sio kama Daudi baba yake alivyokuwa amefanya. Katika kila kitu alifuata mfano wa Yoashi baba yake.
4Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko.
5Baada ya ufalme kuimarika mikononi mwake, aliwaua maafisa waliomuua mfalme baba yake.
6Hata hivyo, hakuwaua wana wa wale wauaji, sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Mose ambako Bwana aliamuru, “Baba hawatauawa kwa ajili ya watoto wao, wala watoto kwa ajili ya baba zao. Kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe.”
7Ndiye aliwashinda Waedomu elfu kumi katika Bonde la Chumvi, na akauteka Sela katika vita, naye akauita Yoktheeli, jina ambalo mji huo unalo hadi leo.