11Mfalme wa Ashuru akawahamishia Waisraeli huko Ashuru na akawaweka Hala, na Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi.
12Hili lilitokea kwa sababu hawakumtii Bwana Mungu wao, lakini walikuwa wamevunja agano lake, yale yote ambayo Mose mtumishi wa Bwana aliwaamuru. Hawakuzisikiliza amri wala kuzitimiza.
13Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka.
14Basi Hezekia mfalme wa Yuda akamtumia ujumbe mfalme wa Ashuru huko Lakishi akisema: “Nimefanya makosa. Ondoka katika nchi yangu, nami nitakulipa chochote unachokitaka kwangu.” Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia mfalme wa Yuda talanta 300 za fedha, na talanta thelathini za dhahabu.
15Basi Hezekia akampa fedha yote iliyopatikana ndani ya Hekalu la Bwana na katika hazina ya jumba la mfalme.