1Neno la Bwana likanijia kusema:
2“Mwanadamu, tabiri juu ya wachungaji wa Israeli, tabiri na uwaambie: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ole wa wachungaji wa Israeli ambao hujitunza wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kutunza kundi la kondoo?
3Mnakula mafuta ya wanyama, mnavaa mavazi ya sufu na kuchinja kondoo walionona, lakini hamlitunzi kundi.
4Hamkuwatia nguvu walio dhaifu wala hamkuwaganga wenye maradhi wala kuwafunga waliojeruhiwa. Hamkuwarudisha waliotangatanga wala kuwatafuta wale waliopotea. Badala yake mmewatawala kwa ukali na kwa ukatili.