20“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi awaambialo: Tazama, mimi mwenyewe nitahukumu kati ya kondoo wanono na waliokonda.
21Kwa sababu mmewapiga kikumbo na kuwapiga kwa pembe zenu kondoo wote walio dhaifu mpaka wakawafukuza,
22nitaliokoa kundi langu na hawatatekwa nyara tena. Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo.
23Nitaweka juu yao mchungaji mmoja, mtumishi wangu Daudi, naye atawachunga, atawachunga na kuwa mchungaji wao.
24Mimi Bwana nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu miongoni mwao. Mimi Bwana nimenena.