1Neno la Bwana likanijia kusema:
2“Mwanadamu, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo kwa nchi ya Israeli: Mwisho! Mwisho umekuja juu ya pembe nne za nchi.
3Sasa mwisho umekuja juu yenu nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu. Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza.
4Sitawaonea huruma wala sitawarehemu, hakika nitalipiza kwa ajili ya matendo yenu na desturi zenu za machukizo miongoni mwenu. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana.