42Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yosefu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake.
43Akampandisha katika gari lake la farasi kama msaidizi wake, watu wakatangulia wakishangilia, wakisema, “Fungueni njia!” Ndivyo Farao alivyomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.
44Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.”
45Farao akamwita Yosefu Safenath-Panea, pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, kuwa mke wake. Ndipo Yosefu akaitembelea nchi yote ya Misri.
46Yosefu alikuwa na miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao mfalme wa Misri. Naye Yosefu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri.