20Basi, enyi wanawake, sikieni neno la Bwana; fungueni masikio yenu msikie maneno ya kinywa chake. Wafundisheni binti zenu kuomboleza; fundishaneni kila mmoja na mwenzake maombolezo.
21Mauti imeingia ndani kupitia madirishani, imeingia kwenye majumba yetu ya fahari; imewakatilia mbali watoto katika barabara na vijana waume kutoka viwanja vya miji.
22Sema, “Hili ndilo asemalo Bwana: “ ‘Maiti za wanaume zitalala kama mavi katika mashamba, kama malundo ya nafaka nyuma ya mvunaji, wala hakuna anayekusanya.’ ”
23Hili ndilo asemalo Bwana: “Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake, au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake, wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,
24lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili: kwamba ananifahamu na kunijua mimi, kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema, hukumu na haki duniani, kwa kuwa napendezwa na haya,” asema Bwana.