8Matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu, machukizo aliyoyafanya na yote yaliyoonekana dhidi yake, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.
9Yehoyakini alikuwa na miaka kumi na minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu na siku kumi. Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana.
10Mnamo majira ya vuli, Mfalme Nebukadneza akatuma watu, nao wakamleta Babeli, pamoja na vyombo vya thamani kutoka Hekalu la Bwana. Naye akamfanya Sedekia, ndugu yake Yehoyakimu kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu.
11Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na mmoja.
12Alifanya maovu machoni pa Bwana Mungu wake, wala hakujinyenyekeza mbele ya nabii Yeremia, ambaye alinena neno la Bwana.