10Ndipo akawapa wale wakuu mikuki na ngao zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana.
11Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.
12Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano, na kumtangaza kuwa mfalme. Wakamtia mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”
13Athalia aliposikia kelele iliyofanywa na walinzi pamoja na watu, akawaendea watu pale penye Hekalu la Bwana.
14Akaangalia, na tazama alikuwako mfalme, akiwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa pembeni mwa mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wakifurahi na kupiga tarumbeta. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”