39“Lakini baba zetu walikataa kumtii Mose, badala yake wakamkataa na kuielekeza mioyo yao Misri tena.
40Wakamwambia Aroni, ‘Tufanyie miungu watakaotuongoza, kwa maana mtu huyu Mose aliyetutoa nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.’
41Huu ni ule wakati walitengeneza sanamu katika umbo la ndama, wakailetea sadaka kufanya maadhimisho kwa ajili ya kile kitu walichokitengeneza kwa mikono yao wenyewe.
42Ndipo Mungu akageuka, akawaacha waabudu jeshi lote la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Manabii: “ ‘Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli?
43La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki, na nyota ya mungu wenu Refani, vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu. Kwa hiyo nitawapeleka mbali’ kuliko Babeli.