18Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi; mkamsahau Mungu aliyewazaa.
19Bwana akaona hili, akawakataa, kwa sababu alikasirishwa na wanawe na binti zake.
20Akasema, “Nitawaficha uso wangu, nami nione mwisho wao utakuwa nini, kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka, watoto ambao si waaminifu.
21Wamenifanya niwe na wivu kwa kile ambacho si mungu, na kunikasirisha kwa sanamu zao zisizokuwa na thamani. Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa. Nitawafanya wakasirishwe na taifa lile lisilo na ufahamu.
22Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu, ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti. Utateketeza dunia pamoja na mazao yake, na kuwasha moto katika misingi ya milima.