28Mose alikuwa huko pamoja na Bwana kwa siku arobaini usiku na mchana bila kula chakula wala kunywa maji. Naye akaandika juu ya vibao maneno ya Agano, yaani zile Amri Kumi.
29Mose alipoteremka kutoka Mlima Sinai akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa ukingʼaa, kwa sababu alikuwa amezungumza na Bwana.
30Aroni na Waisraeli wote walipomwona Mose, kuwa uso wake unangʼaa, waliogopa kumkaribia.
31Lakini Mose akawaita, kwa hiyo Aroni na viongozi wote wa jumuiya wakarudi, naye akazungumza nao.
32Baadaye Waisraeli wote wakamkaribia, naye akawapa amri zote Bwana alizompa katika Mlima wa Sinai.