20Wale maafisa wa Farao ambao waliliogopa neno la Bwana wakafanya haraka kuwaleta watumwa wao na mifugo yao ndani.
21Lakini wale waliopuuza neno la Bwana wakawaacha watumwa wao na mifugo yao shambani.
22Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili kwamba mvua ya mawe inyeshe juu ya Misri yote, juu ya watu, wanyama na juu ya kila kitu kiotacho katika mashamba ya Misri.”
23Mose alipoinyoosha fimbo yake kuelekea angani, Bwana akatuma ngurumo na mvua ya mawe, umeme wa radi ulimulika hadi nchi. Kwa hiyo Bwana akaifanya mvua ya mawe kunyesha juu ya nchi ya Misri,
24mvua ya mawe ikanyesha na radi ikamulika pote. Ikawa dhoruba ya kutisha ambayo haijakuwako katika nchi ya Misri, tangu nchi hiyo iwe taifa.