8Babeli ataanguka ghafula na kuvunjika. Mwombolezeni! Tafuteni zeri ya kutuliza maumivu yake, labda anaweza kupona.
9“ ‘Tungemponya Babeli, lakini hawezi kuponyeka; tumwacheni, na kila mmoja wetu aende nchi yake mwenyewe, kwa kuwa hukumu yake inafika angani, inapanda juu hadi mawinguni.’
10“ ‘Bwana amethibitisha haki yetu; njooni, tutangaze katika Sayuni kitu ambacho Bwana Mungu wetu amefanya.’
11“Noeni mishale, chukueni ngao! Bwana amewaamsha wafalme wa Wamedi, kwa sababu nia yake ni kuangamiza Babeli. Bwana atalipiza kisasi, kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.
12Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli! Imarisheni ulinzi, wekeni walinzi, andaeni waviziao! Bwana atatimiza kusudi lake, amri yake juu ya watu wa Babeli.