25Mashindano yakazuka kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja kuhusu suala la desturi ya kunawa kwa utakaso.
26Wakamwendea Yohana wakamwambia, “Rabi, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ngʼambo ya Mto Yordani, yule uliyeshuhudia habari zake, sasa anabatiza na kila mtu anamwendea!”
27Yohana akawajibu, “Hakuna mtu yeyote awezaye kupata kitu chochote isipokuwa kile tu alichopewa kutoka mbinguni.
28Ninyi wenyewe ni mashahidi wangu kwamba nilisema, ‘Mimi si Kristo, ila nimetumwa nimtangulie.’
29Bibi arusi ni wa bwana arusi. Lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama karibu naye na kusikiliza kutoka kwake, hufurahi sana aisikiapo sauti ya bwana arusi. Kwa sababu hii furaha yangu imekamilika.