20Naye Sisera akamwambia, “Simama mlangoni pa hema na mtu yeyote akija na kukuuliza, ‘Je, kuna mtu yeyote hapa?’ sema, ‘Hapana.’ ”
21Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akachukua nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akiwa amelala usingizi, akiwa amechoka. Akakigongomea kile kigingi kwenye paji la uso wake, kikapenya hata kuingia ardhini, naye akafa.
22Baraka akakaribia akimfuatia Sisera, Yaeli akatoka kumlaki. Akamwambia, “Njoo, nitakuonyesha mtu unayemtafuta.” Hivyo wakaingia ndani ya hema wakiwa wamefuatana na tazama Sisera alikuwa amelala humo, akiwa amekufa, na hicho kigingi cha hema kikiwa kimegongomewa kupitia paji la uso wake.
23Basi siku ile Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani, mbele ya Israeli.
24Nao mkono wa Waisraeli ukaendelea kuwa na nguvu zaidi na zaidi dhidi ya Yabini, mfalme wa Kanaani, mpaka wakamwangamiza.