19Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mti wa mwaloni na kumpa.
20Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.
21Malaika wa Bwana akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa Bwana akatoweka kutoka machoni pake.
22Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa Bwana, akapiga kelele kwa mshangao, akasema, “Ole wangu, Bwana Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso!”
23Lakini Bwana akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”