19Atanyunyiza baadhi ya hiyo damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, ili kuitakasa na kuiweka wakfu kutokana na unajisi wa Waisraeli.
20“Aroni atakapokuwa amemaliza kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, atamleta mbele yule mbuzi aliye hai.
21Aroni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha mbuzi aliye hai na kuungama juu yake uovu wote na uasi wa Waisraeli, yaani dhambi zao zote, ili kuziweka juu ya kichwa cha huyo mbuzi. Atamwachia huyo mbuzi akimbilie jangwani kwa uangalizi wa mtu aliyepewa wajibu huo.
22Yule mbuzi atachukua juu yake dhambi zao zote mpaka mahali pasipo na watu; naye yule mtu atamwachia akimbilie jangwani.
23“Kisha Aroni ataenda ndani ya Hema la Kukutania na kuvua yale mavazi ya kitani aliyoyavaa kabla ya kuingia katika Patakatifu pa Patakatifu, naye atayaacha pale.