10Mmojawapo wa wale watu alipoona, akamwambia Yoabu, “Nimemwona Absalomu akiningʼinia kwenye mti wa mwaloni.”
11Yoabu akamwambia huyo mtu, “Nini! Ulimwona Absalomu? Kwa nini hukumpiga papo hapo mpaka chini? Ndipo ningekupa shekeli kumi za fedha na mkanda wa askari shujaa.”
12Lakini huyo mtu akamjibu Yoabu, “Hata kama ningepimiwa shekeli 1,000 mikononi mwangu, nisingeinua mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Tukiwa tunasikia, mfalme alikuagiza wewe na Abishai pamoja na Itai, akisema, ‘Mlindeni kijana Absalomu kwa ajili yangu.’
13Nami kama ningekuwa nimemtendea kwa hila, na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme, wewe mwenyewe ungejitenga nami.”
14Yoabu akasema, “Mimi sitapoteza muda hapa pamoja nawe.” Hivyo akachukua mikuki mitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu nayo moyoni alipokuwa angali hai akiningʼinia katika ule mwaloni.