14Daudi, akiwa amevaa kisibau cha kitani, alicheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote,
15wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Bwana kwa shangwe na sauti za tarumbeta.
16Ikawa Sanduku la Bwana lilipokuwa linaingia katika Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Bwana, akamdharau moyoni mwake.
17Wakaleta Sanduku la Bwana na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana.
18Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote.