12Baada ya Festo kufanya shauri pamoja na baraza lake, akatangaza, “Wewe umeomba rufaa kwa Kaisari, nako kwa Kaisari utakwenda!”
13Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo.
14Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili shauri la Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani.
15Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake.
16“Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu yeyote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa.