23Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea mvinyo. Ukaisifu miungu ya fedha na dhahabu, ya shaba, chuma, miti na mawe, miungu ambayo haiwezi kuona, au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake.
24Kwa hiyo ameutuma mkono ule ulioandika maneno.
25“Haya ndiyo maneno yaliyoandikwa: mene, mene, tekeli na peresi
26“Hii ndiyo maana ya maneno haya: “Mene: Mungu amezihesabu siku za utawala wako na kuukomesha.
27Tekeli: Wewe umepimwa katika mizani na umeonekana umepungua.