11Ee Bwana, bariki ustadi wake wote, nawe upendezwe na kazi ya mikono yake. Vipige viuno vya wale wainukao dhidi yake; wapige adui zake hata wasiinuke tena.”
12Kuhusu Benyamini akasema: “Mwache mpenzi wa Bwana apumzike salama kwake, kwa maana humkinga mchana kutwa, na yule Bwana ampendaye hupumzika kati ya mabega yake.”
13Kuhusu Yosefu akasema: “Bwana na aibariki nchi yake kwa umande wa thamani kutoka mbinguni juu, na vilindi vya maji vilivyotulia chini;
14pamoja na vitu vilivyo bora sana viletwavyo na jua, na vitu vizuri sana vinavyoweza kutolewa na mwezi;
15pamoja na zawadi bora sana za milima ya zamani na kwa wingi wa baraka za vilima vya milele;