18Ndipo utakaposema, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi ambazo zimetumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ”
19Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, la tatu na yale mengine yote yaliyofuata akiwaambia, “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye.
20Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza, hatimaye, nitakapomwona, huenda atanikubali.”
21Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.
22Usiku ule Yakobo akaamka akawachukua wake zake wawili, watumishi wake wawili wa kike na wanawe kumi na mmoja na akavuka kivuko cha Yaboki.