12Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema yalikuwa malipo yake kutoka kwa wapenzi wake; nitaifanya kuwa kichaka, nao wanyama pori wataila.
13Nitamwadhibu kwa ajili ya siku alizowafukizia uvumba Mabaali; alipojipamba kwa pete na kwa vito vya thamani, na kuwaendea wapenzi wake, lakini mimi alinisahau,” asema Bwana.
14“Kwa hiyo sasa nitamshawishi; nitamwongoza hadi jangwani na kuzungumza naye kwa upole.
15Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu, nami nitalifanya Bonde la Akori mlango wa matumaini. Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake, kama siku zile alizotoka Misri.
16“Katika siku ile,” asema Bwana, “utaniita mimi ‘Mume wangu’; hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu.’