6Oeni wake na mzae wana na binti, waozeni wana wenu wake, nanyi watoeni binti zenu waolewe, ili nao pia wazae wana na binti. Ongezekeni idadi yenu huko, wala msipungue.
7Pia tafuteni amani na mafanikio ya mji ambamo nimewapeleka uhamishoni. Mwombeni Bwana kwa ajili ya mji huo, kwa sababu ukistawi, ninyi pia mtastawi.”
8Naam, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: “Msikubali manabii na wabashiri walioko miongoni mwenu wawadanganye. Msisikilize ndoto ambazo mmewatia moyo kuota.
9Wanawatabiria ninyi uongo kwa jina langu. Sikuwatuma,” asema Bwana.
10Hili ndilo asemalo Bwana: “Miaka sabini itakapotimia kwa ajili ya Babeli, nitakuja kwenu na kutimiza ahadi yangu ya rehema ya kuwarudisha mahali hapa.