3Bwana alitutokea wakati uliopita, akisema: “Nimekupenda kwa upendo wa milele, nimekuvuta kwa wema.
4Nitakujenga tena nawe utajengeka upya, ewe Bikira Israeli. Utachukua tena matari yako na kwenda kucheza na wenye furaha.
5Utapanda tena shamba la mizabibu juu ya vilima vya Samaria, wakulima watapanda na kufurahia matunda yake.
6Itakuja siku wakati walinzi watakapowapigia kelele juu ya vilima vya Efraimu wakisema, ‘Njooni, twendeni juu Sayuni, kwake Bwana Mungu wetu.’ ”
7Hili ndilo asemalo Bwana: “Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mpigieni kelele aliye mkuu wa mataifa. Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme, ‘Ee Bwana, okoa watu wako, mabaki ya Israeli.’