25Bwana amefungua ghala lake la silaha na kuzitoa silaha za ghadhabu yake, kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mwenye Nguvu Zote anayo kazi ya kufanya katika nchi ya Wakaldayo.
26Njooni dhidi yake kutoka mbali. Zifungueni ghala zake za nafaka; mlundikeni kama lundo la nafaka. Mwangamizeni kabisa na msimwachie mabaki yoyote.
27Waueni mafahali wake wachanga wote; waacheni washuke machinjoni! Ole wao! Kwa kuwa siku yao imewadia, wakati wao wa kuadhibiwa.
28Wasikilizeni watoro na wakimbizi kutoka Babeli wakitangaza katika Sayuni jinsi Bwana, Mungu wetu alivyolipiza kisasi, kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.
29“Waiteni wapiga mishale dhidi ya Babeli, wote wale wavutao upinde. Pigeni kambi kumzunguka kabisa, asitoroke mtu yeyote. Mlipizeni kwa matendo yake; mtendeeni kama alivyotenda. Kwa kuwa alimdharau Bwana, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.