11Ee Bwana, nifundishe njia yako, nami nitakwenda katika kweli yako; nipe moyo usiositasita, ili niweze kulicha jina lako.
12Ee Bwana wangu, nitakusifu kwa moyo wote; nitaliadhimisha jina lako milele.
13Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu; umeniokoa kutoka kwenye vilindi vya kaburi.
14Ee Mungu, wenye majivuno wananishambulia; kundi la watu wakatili linatafuta uhai wangu: watu wasiokuheshimu wewe.
15Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu.