5Eneo la urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000 litakuwa la Walawi wale wanaotumika hekaluni, kama milki yao kwa ajili ya miji ya kuishi.
6“ ‘Utatoa mji kama mali yao wenye upana wa dhiraa 5,000 na urefu wa dhiraa 25,000, karibu na sehemu takatifu, itakuwa mali ya nyumba yote ya Israeli.
7“ ‘Mkuu anayetawala atakuwa na lile eneo linalopakana na lile eneo lililowekwa wakfu upande huu na upande huu na eneo la mji. Eneo la mji litaenea upande wa magharibi kuanzia upande wa magharibi na upande wa mashariki kuanzia upande wa mashariki, likiendelea kwa urefu kutoka magharibi hadi mpaka wa mashariki sambamba na mojawapo ya sehemu za makabila.
8Nchi hii itakuwa milki yake katika Israeli. Nao wakuu wangu hawataonea tena watu wangu bali watairuhusu nyumba ya Israeli kuimiliki nchi kulingana na makabila yao.
9“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Yatosha, enyi wakuu wa Israeli! Acheni mbali ukatili wenu na uonevu wenu mkafanye lile lililo haki na sawa. Acheni kuwatoza watu wangu isivyo haki, asema Bwana Mwenyezi.