10Tazameni, Bwana Mwenyezi anakuja na nguvu, nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake. Tazameni, ujira wake u pamoja naye, nayo malipo yake yanafuatana naye.
11Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo: Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake na kuwachukua karibu na moyo wake, huwaongoza taratibu wale wanyonyeshao.
12Ni nani aliyepima maji ya bahari kwenye konzi ya mkono wake, au kuzipima mbingu kwa shibiri yake? Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu, au kupima milima kwenye kipimio na vilima kwenye mizani?
13Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana, au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?
14Ni nani ambaye Bwana ametaka shauri kwake ili kumwelimisha, naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa? Ni nani aliyemfundisha maarifa au kumwonyesha mapito ya ufahamu?