27Ikawa Yesu alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya ule umati wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”
28Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”
29Umati wa watu ulipokuwa unazidi kuongezeka, Yesu akaendelea kusema, “Hiki ni kizazi kiovu. Kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.
30Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki.
31Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kuwahukumu watu wa kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.