33Wale watu wakalipokea jambo lile kama dalili nzuri nao wakawa wepesi kulichukua neno lake wakisema, “Ndiyo, yeye ni ndugu yako Ben-Hadadi!” Mfalme akawaambia, “Nendeni mkamlete.” Ikawa Ben-Hadadi alipokuja, Ahabu akampandisha katika gari lake la vita. Ben-Hadadi akajitolea, akisema,
34“Nitairudisha ile miji ambayo baba yangu aliiteka kutoka kwa baba yako. Unaweza kuweka maeneo yako ya soko katika Dameski, kama baba yangu alivyofanya huko Samaria.” Ahabu akasema, “Katika misingi ya mkataba, nitakuachilia huru.” Kwa hiyo akaweka mkataba naye, akamruhusu aende zake.
35Kwa neno la Bwana, mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake, “Nipige kwa silaha yako,” lakini yule mtu akakataa.
36Kwa hiyo yule nabii akasema, “Kwa sababu hukumtii Bwana, mara tu tutakapoachana utauawa na simba.” Na baada ya yule mtu kuondoka, simba akatokea na kumuua.
37Nabii akamkuta mtu mwingine na kumwambia, “Nipige tafadhali.” Kisha yule mtu akampiga na kumjeruhi.